hakimadini

Wednesday, May 03, 2006

From: "amani mustafa"


Date: 3 May 2006
To: pm@pmo.go.tz
Cc: ps@pmo.go.tz, info@pmotz.org
Subject: barua ya wazi kwa Mhe Lowassa-Uchunguzi Mererani



Kwako Mhe Lowassa
Kutokana na habari zilizonukuliwa magazetini na malalamiko yanayomgusa Mhe Lawrence Masha..naibu Waziri wa Madini na Mkurugenzi wa AFGEM,uzalendo umenishinda.
Ndugu Waziri Mkuu,tunashukuru kuwa uliagiza Waziri husika na Madini kutembelea Mererani baada ya malalamiko ya wana-Mererani hivi majuzi ulipokuja kwa ziara ya kikazi.Hii yote ilitokana na uchungu ulionao kuona uozo ulioko katika sekta ya madini unaondoka kabisa.Mhe Rais pia, amesisitiza azma yake kuondoa kero zote zilizoko katika sekta ya madini ili kuleta manufaa ya kweli katika eneo hili.
Mhe Waziri Mkuu,tatizo la Mererani sio geni kwani tangu serikali ya awamu ya pili kulikuwa na vijimambo.Ila katika awamu ya tatu,ndio mwanzo wa mpasuko huu mkubwa wa kijamii na kiuchumi sio tu Mererani bali hata Machimbo ya dhahabu Geita,Bulyanhulu na Nyamongo-Tarime.
Kwa kweli nafikiri tofauti na Bulyanhulu sehemu iliundiwa tume na kamati nyingi zaidi za uchunguzi ni Mererani.Mhe.Waziri Mkuu,pamoja na maagizo yako yenye nia nzuri kumuuagiza Mhe Dr Msabaha kuja Mererani kusikiliza kero za wananchi,zoezi hili limegubikwa na
walakin!!
Waziri husika badala ya kuja mwenyewe aliagiza maafisa wake kuja kukusanya maoni ya wadau kuhusu tatizo la Mererani.Watendaji hawa ndio wale wale ambao wamekuwa miaka nenda rudi wakipuuzia malalamiko ya wananchi na hata kutoa vitisho kwa wanaonyesha uzalendo wao.Watu hawa hawana dhamira ya kweli ya kutatua tatizo hili,bali ndio walewale wanaolea uchafu huu.Wala sioni kama wana jipya..tumewazoea walivyo.Naomba kuorodhesha mapungufu ya uchunguzi wao na yanayokatisha tamaa ifuatayo..

a)Hawakuzingatia utawala bora kwani Watumishi hawa hawakuwa na ratiba iwe ya maandishi au kauli kuhusu wapi watakapokuwa,lini watakuwepo,nani watakutana nao,lipi litajadiliwa..Hii ilitakiwa kila mwananchi aliye mdau na kero alifahamu angalau siku mbili kabla.

b)Hawakushirikisha wadau wa tanzanite kwa dhana pana ya ushirikishwaji.Wala sijui kama wanafahamu wadau ni akina nani?Tabia ile ile ya kuwachukulia kuwa wenye leseni ya kuchimba na wanunuzi wakubwa(master dealers)peke yao ndio wadau wa Tanzanite ni dhana
muflis inayozaa majungu na fujo.Hebu fikiria mamlaka inayosimamia ardhi chini ya Sheria ya ardhi ya vijiji 1999 hazikuhusishwa,hivi serikali hadi ngazi ya wilaya Simanjiro(tofauti na DC binafsi) zipo kwa maandishi tu au ni ya kweli,au wafugaji ambao maeneo yao ya malisho yamechukuliwa kibabe au akina mama wanaofanya kazi kutoa huduma ndani ya eneo hilo sio wadau!!
Kwa mtu yeyote anayeenda kufanya utafiti/uchunguzi/upembuzi ni lazima awe na mwongozo kuhusu wadau(inventory),atakavyowafikia na kuwahusisha kuhusu maslahi yao.

C)Hawa watu walikuja Mererani na Arusha wakiwa na mawazo yaliyojengeka awali(fixed mind).Waliokutana nao(japo wachache)walionyeshwa kukatishwa tamaa na mazungumzo yao.Lengo lao ilikuwa kutafuta wachawi kwa lengo la kuwaridhisha mabwana zao.Mi sitashangaa ripoti hiyo ya Waziri wa Madini kwako ikisema hamna tatizo ili ni wachochezi wachache na wavuta bangi tu au kuna kikundi kinacholipwa ili kuchochea vurugu na matajiri fulani!!Ripoti ya Meja Jenerali(mstaafu)Mangenya iliwataja watu wa Mererani majina ya aina hii pia mwaka 2000.
Yale yale mpe mbwa jina baya ili umuue kirahisi!!

Ndugu Waziri Mkuu,serikali yako haihitaji mambo kufanyika kwa uficho au kuogopana kwenye maslahi ya taifa.Mazoea ya watendaji miaka iliyopita isiwe kikwazo kwa serikali yako hii iliyopewa nafasi kubwa kuwatetea wanyonge.
Mhe Waziri Mkuu,sioni haja ya kufanya uchunguzi mwingine wa warasimu hawa,utakaotumia hela nyingi za wafuja jasho!!Mwaka juzi wakati wa bajeti ya Wizara ya nishati na madini 2004/05,Bunge letu tukufu lilimuunga mkono Mbunge(zamani)Mhe Parsenko Kone kwa kuazimia
kuunda kamati ya Bunge kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu na kero za Mererani.
Uamuzi huu wa Bunge letu tukufu,uliuawa kikatili ndani na nje ya Bunge!!Kuna maelezo mengi sana kuhusu kilichotokea baada ya hapo ndani ya taratibu za Bunge!!Ila tunafahamu aliyefanya hivyo alitaka kuficha ukweli kwa njia ile ile walivyozuia ripoti ya Tume ya
Uchunguzi ya Jenerali (mstaafu)Robert Mboma 2002.

Mhe Waziri Mkuu tatizo liko Mererani na litaendelea kuwepo kama hatua za dhati hazitachukuliwa na wapenda amani na heshima ya taifa letu.Inashangaza kuwa kuna viongozi ambao wanahoji uzalendo wa Watanzania waliokuita siku ile Mererani kukuelezea kero zao.Hawa
ni viongozi ambao wamekuwa kwa muda mrefu wakijaribu kunyamazisha kilio cha wanyonge!!!
Wizara ya Nishati na Madini halina jipya,na ndio maana tunaomba kupitia kwako kama kiongozi ya serikali Bungeni kutuletea kamati ya Bunge.Wabunge wasiofungamana na upande wowote,walio na uchungu na
nchi yao!!Ila uchunguzi huu wa Wizara ya madini hadi sasa ni usanii kwa kweli!!

AMANI MUSTAFA MHINDA
(Mwanasheria na Mwanaharakati wa haki za binadamu)

COORDINATOR-Non profit making organisation
TANZANIA MINEWORKERS DEVELOPMENT ORGANISATION
P.O BOX 12536 ARUSHA
Physical Address:CCM Stadium Building Mererani
Simanjiro

0 Comments:

Post a Comment

<< Home